Mithali Chapter 21
1
Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa Bwana; Kama mifereji ya maji huugeuza po pote apendapo.
2
Kila njia ya mtu ni sawa machoni pake mwenyewe; Bali Bwana huipima mioyo.
3
Kutenda haki na hukumu Humpendeza Bwana kuliko kutoa sadaka.
4
Macho yenye kiburi, na moyo wa kutakabari, Hata ukulima wa waovu, ni dhambi.
5
Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu; Bali kila mwenye pupa huuelekea uhitaji.
6
Kupata akiba ya mali kwa ulimi wa uongo Ni moshi upeperushwao; ni kutafuta mauti.
7
Jeuri ya wabaya itawaondolea mbali; Kwa sababu wamekataa kutenda hukumu.
8
Njia yake aliyelemewa na dhambi imepotoka sana; Bali mtu aliye safi, kazi yake ni sawasawa.
9
Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi.
10
Nafsi ya mtu mbaya hutamani uovu; Jirani yake hapati fadhili machoni pake.
11
Mwenye mzaha aadhibiwapo, mjinga hupata hekima; Na mwenye hekima afundishwapo, hupokea maarifa.
12
Mwenye haki huitafakari nyumba ya mtu mbaya; Jinsi wabaya waangushwavyo wakaangamia.
13
Azibaye masikio yake asisikie kilio cha maskini, Yeye naye atalia, lakini hatasikiwa.
14
Kipawa cha siri hutuliza hasira; Na rushwa bindoni humliza ghadhabu kali.
15
Ni furaha yao wenye haki kutenda hukumu; Lakini ni uharibifu kwao watendao maovu.
16
Mtu aikosaye njia ya busara Atakaa katika mkutano wao waliokufa.
17
Mtu apendaye anasa atakuwa maskini; Apendaye mvinyo na mafuta hatakuwa tajiri.
18
Mtu asiye haki ni fidia ya wenye haki; Naye afanyaye hila ni badala ya watu wa adili.
19
Ni afadhali kukaa katika nchi ya nyika; Kuliko na mwanamke mgomvi, mchokozi.
20
Kuna hazina ya thamani na mafuta katika maskani ya mwenye hekima; Bali mwanadamu aliye mpumbavu huyameza.
21
Aandamaye haki na fadhili, Ataona uhai na haki na heshima.
22
Mwenye hekima huupandia mji wao wenye nguvu; Na kuziangusha nguvu za tumaini lao.
23
Mtu azuiaye kinywa chake na ulimi wake, Atajilinda nafsi yake na taabu.
24
Mwenye kiburi na kutakabari, jina lake ni mbishi; Hutenda mambo katika majivuno ya kiburi chake.
25
Matakwa yake mtu mvivu humfisha, Kwa maana mikono yake hukataa kufanya kazi.
26
Kuna atamaniye kwa choyo mchana kutwa; Bali mwenye haki hutoa wala hanyimi.
27
Sadaka ya wasio haki ni chukizo; Si zaidi sana ailetapo mwenye nia mbaya!
28
Shahidi wa uongo atapotea; Bali mtu asikiaye atasema maneno yadumuyo.
29
Asiye haki huufanya uso wake kuwa mgumu; Bali mtu mnyofu huzifikiri njia zake.
30
Hapana hekima, wala ufahamu, Wala shauri, juu ya Bwana.
31
Farasi huwekwa tayari kwa siku ya vita; Lakini Bwana ndiye aletaye wokovu.