Zaburi Sura 30
1
Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua, Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu.
2
Ee Bwana, Mungu wangu, Nalikulilia ukaniponya.
3
Umeniinua nafsi yangu, Ee Bwana, kutoka kuzimu. Umenihuisha na kunitoa Miongoni mwao washukao shimoni.
4
Mwimbieni Bwana zaburi, Enyi watauwa wake. Na kufanya shukrani. Kwa kumbukumbu la utakatifu wake.
5
Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo, Katika radhi yake mna uhai. Huenda kilio huja kukaa usiku, Lakini asubuhi huwa furaha.
6
Nami nilipofanikiwa nalisema, Sitaondoshwa milele.
7
Bwana, kwa radhi yako Wewe uliuimarisha mlima wangu. Uliuficha uso wako, Nami nikafadhaika.
8
Ee Bwana, nalikulilia Wewe, Naam, kwa Bwana naliomba dua.
9
Mna faida gani katika damu yangu Nishukapo shimoni? Mavumbi yatakusifu? Yataitangaza kweli yako?
10
Ee Bwana, usikie, unirehemu, Bwana, uwe msaidizi wangu.
11
Uligeuza matanga yangu kuwa machezo; Ulinivua gunia, ukanivika furaha.
12
Ili utukufu wangu ukusifu, Wala usinyamaze. Ee Bwana, Mungu wangu, Nitakushukuru milele.