Zaburi Chapter 86
1
Ee Bwana, utege sikio lako unijibu, Maana mimi ni maskini na mhitaji
2
Unihifadhi nafsi yangu, Maana mimi ni mcha Mungu. Wewe uliye Mungu wangu, Umwokoe mtumishi wako anayekutumaini.
3
Wewe, Bwana, unifadhili, Maana nakulilia Wewe mchana kutwa.
4
Uifurahishe nafsi ya mtumishi wako, Maana nafsi yangu nakuinulia Wewe, Bwana.
5
Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema, Umekuwa tayari kusamehe, Na mwingi wa fadhili, Kwa watu wote wakuitao.
6
Ee Bwana, uyasikie maombi yangu; Uisikilize sauti ya dua zangu.
7
Siku ya mateso yangu nitakuita, Kwa maana utaniitikia.
8
Katikati ya miungu hakuna kama Wewe, Bwana, Wala matendo mfano wa matendo yako.
9
Mataifa yote uliowafanya watakuja; Watakusujudia Wewe, Bwana, Watalitukuza jina lako;
10
Kwa kuwa ndiwe uliye mkuu, Wewe ndiwe mfanya miujiza, Ndiwe Mungu peke yako.
11
Ee Bwana, unifundishe njia yako; Nitakwenda katika kweli yako; Moyo wangu na ufurahi kulicha jina lako;
12
Nitakusifu Wewe, Bwana, Mungu wangu, Kwa moyo wangu wote, Nitalitukuza jina lako milele.
13
Maana fadhili zako kwangu ni nyingi sana; Umeiopoa nafsi yangu na kuzimu.
14
Ee Mungu, wenye kiburi wamenishambulia; Mkutano wa wakatili wamenitafuta roho. Wala hawakukuweka Wewe Mbele ya macho yao.
15
Lakini Wewe, Bwana, U Mungu wa rehema na neema, Mvumilivu, mwingi wa fadhili na kweli.
16
Unielekee na kunifadhili mimi; Mpe mtumishi wako nguvu zako, Umwokoe mwana wa mjakazi wako.
17
Unifanyie ishara ya wema, Wanichukiao waione na kuaibishwa. Kwa kuwa Wewe, Bwana, Umenisaidia na kunifariji.