Zaburi Chapter 98
1
Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Kwa maana ametenda mambo ya ajabu. Mkono wa kuume wake mwenyewe, Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
2
Bwana ameufunua wokovu wake, Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
3
Amezikumbuka rehema zake, Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu.
4
Mshangilieni Bwana, nchi yote, Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi.
5
Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi, Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
6
Kwa panda na sauti ya baragumu. Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana.
7
Bahari na ivume na vyote viijazavyo, Ulimwengu nao wanaokaa ndani yake.
8
Mito na ipige makofi, Milima na iimbe pamoja kwa furaha.
9
Mbele za Bwana; Kwa maana anakuja aihukumu nchi. Atauhukumu ulimwengu kwa haki, Na mataifa kwa adili.