Zaburi Sura 58
1
Ni kweli, enyi wakuu, mnanena haki? Enyi wanadamu, mnahukumu kwa adili?
2
Sivyo! Mioyoni mwenu mnatenda maovu; Katika nchi mnapima udhalimu wa mikono yenu.
3
Wasio haki wamejitenga tangu kuzaliwa kwao; Tangu tumboni wamepotea, wakisema uongo.
4
Sumu yao, mfano wake ni sumu ya nyoka; Mfano wao ni fira kiziwi azibaye sikio lake.
5
Asiyeisikiliza sauti ya waganga, Ijapo wanafanya uganga kwa ustadi.
6
Ee Mungu, uyavunje meno yao vinywani mwao; Ee Bwana, uyavunje magego ya wana-simba.
7
Na watoweke kama maji yapitayo kwa kasi; Akiielekeza mishale yake, iwe imetiwa ubutu.
8
Kama konokono ayeyukaye na kutoweka, Kama mimba iliyoharibika, isiyoliona jua,
9
Kabla ya masufuria yenu kupata moto wa miiba, Ataipeperusha kama chamchela, Iliyo mibichi na iliyo moto.
10
Mwenye haki atafurahi akionapo kisasi; Ataiosha miguu yake katika damu ya wasio haki.
11
Na mwanadamu atasema, Hakika iko thawabu yake mwenye haki. Hakika yuko Mungu Anayehukumu katika dunia.